Jinsi ya Kukata Rufaa
Uwasilishaji wa Malalamiko au Rufaa
Rufaa : Maana yake ni mchakato unaomuwezesha mzabuni ambaye hajaridhika na uamuzi, suala, kitendo au kutokutenda kwa afisa masuuli wa taasisi nunuzi au kufungiwa kwa mzabuni na Mamlaka kupata nafuu ya kisheria.
Malalamiko: Maana yake ni malalamiko yanayowasilishwa na mzabuni kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 112 (6) cha Sheria.
A :Uwasilishaji wa Rufaa
- Iwapo Mzabuni aliwasilisha malalamiko yake kwa Afisa Masuuli kwa mujibu wa taratibu na hajaridhishwa na uamuzi uliotolewa na Afisa Masuuli juu ya lalamiko lake, Mzabuni anaweza kuwasilisha rufaa mbele ya Mamlaka ya Rufani ndani ya siku tano (5) za kazi toka alipofahamu jambo au uamuzi anaoulalamikia.
- Mzabuni ambaye hajaridhika na uamuzi wa PPRA wa kumfungia kushiriki katika zabuni za umma, anaweza kuwasilisha rufaa mbele ya Mamlaka ya Rufani ndani ya siku ishirini na moja kuanzia tarehe alipofahamu kuwepo kwa uamuzi huo wa kumfungia.
Mzabuni awasilishe Rufaa yake kwa kujaza PPAA Fomu Na. 1 ambayo ni Hati ya Rufaa ( Bonyeza kupakua PPAA Fomu 1) pamoja na kulipa ada ya Rufaa (Bonyeza kuona gharama). Mamlaka ya Rufani itatakiwa kutoa uamuzi wake ndani ya siku arobaini (40) tangu kusajiliwa kwa Rufaa.
B: Uwasilishaji wa Malalamiko
- Iwapo Afisa Masuuli hajatoa uamuzi wake ndani ya muda wa siku tano (5) za kazi, mzabuni anaweza kuwasilisha malalamiko mbele ya Mamlaka ya Rufani ndani ya siku tano (5) za kazi tangu tarehe ambayo Afisa masuuli alipaswa kutoa uamuzi.
- Kama mkataba umesainiwa, Mzabuni atawasilisha malalamiko yake moja kwa moja mbele ya Mamlaka ya Rufani ndani ya siku tano (5) za kazi tangu alipofahamu jambo analolilalamikia.
Mzabuni awasilishe Malalamiko yake kwa kujaza PPAA Fomu Na. 1 ambayo ni Hati ya Rufaa (Bonyeza kupakua PPAA Fomu 1) pamoja na kulipa ada ya Rufaa (Bonyeza kuona gharama). Mamlaka ya Rufani itatakiwa kutoa uamuzi wake ndani ya siku arobaini (40) tangu kusajiliwa kwa Malalamiko.
ANGALIZO:
- Zingatia ukomo wa muda wa uwasilishaji wa Malalamiko au Rufaa mbele ya Mamlaka ya Rufani.
- Mamlaka ya Rufani haishughulikii Malalamiko yatokanayo na utekelezaji wa mkataba.
Mambo yanayoweza kulalamikiwa: -
- Kukubaliwa au Kukataliwa kwa Zabuni;
- Tuzo au kusudio la kutoa tuzo;
- Vipengele visivyokubalika kwenye kabrasha la zabuni;
- Mchakato wa Zabuni usiozingatia taratibu;
- Kushindwa au kutokutoa uamuzi ndani ya muda uliowekwa; na
- Kufungiwa kwa Mzabuni na Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA)
Mawasiliano: -
Katibu Mtendaji,
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma,
S.L.P 1385,
Dodoma.
Barua pepe: es@ppaa.go.tz au barua@ppaa.go.tz
TAARIFA ZA KUWASILISHA
Jina na anwani ya Wizara au Taasisi Nunuzi iliyotangaza zabuni inayolalamikiwa.
Zabuni inayolalamikiwa.
Sababu zinazopelekea rufaa / malalamiko.
Nafuu zinazoombwa.
Kujiunga katika Shauri
Mzabuni mwenye maslahi katika Rufaa iliyowasilishwa (Mzabuni anayekusudiwa kupewa tuzo) anaweza kujiunga kama mhusika katika shauri ndani ya siku tano za kazi tangu kupokea taarifa juu ya uwepo wa shauri. Mhusika anaweza kujiunga katika shauri kwa kuwasilisha Fomu ya PPAA Na. 5 (Fomu ya PPAA 5) kwa mujibu wa Kanuni ya 17 ya Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma. Bofya hapa Kupakua Fomu na Bofya hapa kuangalia ada husika