Hstoria ya PPAA
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) ni Taasisi ya Serikali inayojitegemea chini ya Wizara ya Fedha.
Mamlaka ya Rufani iliundwa kwa Mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.3 ya Mwaka 2001 ambapo baada ya Sheria hiyo kufutwa, Mamlaka ya Rufani iliendelezwa chini ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 21 ya mwaka 2004.
Mwaka 2011 Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 21 ya mwaka 2004 ilifutwa na Mamlaka ya Rufani iliendelea kuhuishwa kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011. Mwaka 2023 Mamlaka ya Rufani ilihuishwa tena kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023 iliyofuta Sheria Na. 7 ya Mwaka 2011.
DHUMUNI LA KUANZISHWA KWA MAMLAKA YA RUFANI (PPAA)
Dhumuni la kuanzishwa kwa Mamlaka ya Rufani ni kuwa na chombo mbadala cha kutatua migogoro itokanayo na michakato ya ununuzi wa Umma kwa muda mfupi zaidi tofauti na Mahakama za kawaida ili kutochelewesha utekelezaji wa shughuli, huduma na miradi ya Serikali na kuhakikisha uzingatiaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Mamlaka pia husimamia utawala bora kupitia utatuzi wa migogoro inayowasilishwa mbele yake kwa kuhakikisha kuwa zabuni zinatolewa kwa wazabuni wenye sifa stahiki za kufanya kazi husika na hivyo kuwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zake katika ununuzi wa Umma.